Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Kukatwa Kichwa kwa Yohane Mbatizaji (Alhamisi, Agosti 29, 2024)  

Somo la 1

1Kor 1:1–9

Paulo, aliyeitwa kuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu, na Sosthene ndugu yetu, kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu. Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kwa sababu ya neema ya Mungu mliyopewa katika Kristo yesu; kwa kuwa katika kila jambo mlitajirika katika yeye, katika maneno yote, na maarifa yote; kama ushuhuda wa Kristo ulivyothibitika kwenu; hata hamkupungukiwa na karama yoyote, mkikutazamia sana kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye atawathibitisha hata mwisho, ili msilaumiwe siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingine katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu.

Wimbo wa Katikati

Zab 145:2–7

Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.
Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana,
Wala ukuu wake hautambulikani.
(K) Ee Bwana, nitalihimidi jina lako milele na milele.

Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako,
Kitayatangaza matendo yako makuu.
Nitakufikiri fahari ya utukufu wa adhama yako,
Na matendo yako yote ajabu
(K) Ee Bwana, nitalihimidi jina lako milele na milele.

Watu watayajua matendo yako ya kutisha,
Nami nitausimulia ukuu wako.
Watalihubiri kumbukumbu la wema wako mkuu.
Wataiimba haki yako.
(K) Ee Bwana, nitalihimidi jina lako milele na milele.

Shangilio

Yn 14:23

Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda, na sisi tutakuja kwake.
Aleluya.

Injili

Mt 24:42–51

Yesu aliwambia wanafunzi wake: Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja. Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Maoni


Ingia utoe maoni