Masomo ya Misa
Jumatatu ya 21 ya Mwaka (Jumatatu, Agosti 26, 2024)
2The 1:1-5, 11-12
Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba yetu, na Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana Yesu Kristo. Ndugu, imetupasa kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kama ilivyo wajibu, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa kila mtu kwenu kwa mwenzake umekuwa mwingi. Hata na sisi wenyewe twaona fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya saburi yenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na dhiki mnazostahimili. Ndiyo ishara hasa ya hukumu iliyo haki ya Mungu, ili mhesabiwe kuwa mwastahili kuuingia ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili yake mnateswa. Kwa hiyo twawaombea ninyi sikuzote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu; jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.
Zab 96:1-5
Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake,
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake.
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake
Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana. Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
Maana miungu yote ya watu si kitu, Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake
Yn 10:27
Aleluya, aleluya
Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya
Mt 23:13-22
Yesu aliwaambia makutano na wafuasi wake:Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie. [Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi.] Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe. Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga. Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au lile hekalu liitakasalo dhahabu? Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga. Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka? Basi yeye aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo juu yake. Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake. Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake.
Maoni
Ingia utoe maoni