Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 21 ya Mwaka (Jumapili, Agosti 25, 2024)  

Somo la 1

Yos 24: 1-2, 15-18

Yoshua aliwakusanya kabila zote za Israeli huko Shekemu, akawaita wazee wa Israeli, na wakuu wao, na waamuzi wao, na maakida yao; na wakahudhuria mbele za Mungu. Yoshua akawaambia watu wote, Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nvumba yangu tutamtumikia Bwana. Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine; kwa maana Bwana, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiya aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao. Basi, kwa sababu hiyo sisi nasi tutamtumikia Bwana; maana yeye ndiye Mungu wetu.

Wimbo wa Katikati

Zab. 34:1-2, 15-22

Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wenyenyekevu wasikie wakafurahi.
(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema.

Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,
Na masikio yake hukielekea kilio chao.
Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema.

Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote.
Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema.

Mateso ya mwenye haki ni mengi,
Lakini Bwana humponya nayo yote.
Huihifadhi mifupa yake yote,
Haukuvunjika hata mmoja.
(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema.

Uovu utamwua asiye haki,
Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa,
Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake,
Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao.
(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema.

Somo la 2

Efe 5: 21-32

Hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo. Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo, bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. .Maana hakuna mtu anayechukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa.

Shangilio

Yn. 14: 23

Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu; Na Baba yangu atampenda; Nasi tutakuja kwake.
Aleluya.

Injili

Yn. 6: 60-69

Watu wengi miongoni mwa wanafunzi wa Yesu waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia? Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung’unikia neno hilo, akawaambia, Je! neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.

Maoni


Ingia utoe maoni