Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 20 ya Mwaka (Ijumaa, Agosti 23, 2024)  

Somo la 1

Eze 37:1-14

Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana. Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe. Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la Bwana. Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi. Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. Basi nikatoa unabii kama nilivyoamriwa; hata nilipokuwa nikitoa unabii, palikuwa na mshindo mkuu; na tazama, tetemeko la nchi, na ile mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe. Nikatazama, kumbe! Kulikuwa na mishipa juu yake, nyama ikatokea juu yake, ngozi ikaifunika juu yake; lakini haikuwamo pumzi ndani yake. Ndipo akaniambia, Tabiri, utabirie upepo, mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana MUNGU asema hivi; Njoo, kutoka pande za pepo nne, Ee pumzi, ukawapuzie hawa waliouawa, wapate kuishi. Basi nikatabiri kama alivyoniamuru; pumzi ikawaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno. Kisha akaniambia, Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa. Basi tabiri, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu, enyi watu wangu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo, na kuyatimiza, asema Bwana.

Wimbo wa Katikati

Zab 107:2-9

Na waseme hivi waliokombolewa na Bwana, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi.
Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni Mwema. Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa.
Waliona njaa, waliona na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni Mwema. Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.
Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni Mwema. Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Na wamshukuru Bwana, kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.
Maana hushibisha nafsi yenye shauku, Na nafsi yenye njaa huijaza mema.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni Mwema. Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Shangilio

Zab 25:4b, 5a

Aleluya, aleluya
Unifundishe mapito yako, Uniongoze katika kweli yako,
Aleluya

Injili

Mt 22:34-40

Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii

Maoni


Ingia utoe maoni