Masomo ya Misa
Jumanne ya 20 ya Mwaka (Jumanne, Agosti 20, 2024)
Eze 28:1–10
Neno la Bwana likanijia tena, kusema, Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana mungu asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu. Tazama, una hekima kuliko Danieli; hapana neno la siri watu wawezalo kukuficha; kwa hekima yako na kwa fahamu zako umejipatia utajiri, nawe umepata dhahabu na fedha katika hazina zako; kwa hekima yako nyingi, na kwa biashara yako, umeongeza utajiri wako, moyo wako umeinuka kwa sababu ya utajiri wako. Basi, kwa hiyo, Bwana Mungu asema hivi; Kwa kuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu; basi, tazama, nitaleta wageni juu yako, watu wa mataifa wenye kutisha; nao watafuta panga zao juu ya uzuri wa hekima yako, nao watautia uchafu mwangaza wako. Watakushusha hata shimoni; nawe utazidi kusema mbele yake huyo akuuaye, Mimi ni Mungu? Lakini u mwanadamu, wala si Mungu, mkononi mwake akutiaye jeraha. Utakufa kifo cha hao wasiotahiriwa, kwa mikono ya wageni; kwa maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana Mungu.
Kum 32:26–28, 30, 35–36
Nalisema, Ningewatawanyia mbali,
Ningekomesha kumbukumbu lao kati ya wanadamu;
Isipokuwa naliogopa makamio ya adui,
Adui zao wasije wakafikiri uongo.
(K) Naua Mimi, nahuisha Mimi.
Wasije wakasema, Mkono wetu umetukuka,
Wala Bwana hakuyafanya haya yote.
Maana hawa ni taifa wasio shauri,
Wala fahamu hamna ndani yao.
(K) Naua Mimi, nahuisha Mimi.
Mmoja angefukuzaje watu elfu,
Wawili wangekimbizaje elfu kumi,
Kama Mwamba wao asingaliwauza,
Kama Bwana asingaliwatoa?
(K) Naua Mimi, nahuisha Mimi.
Mmoja angefukuzaje watu elfu,
Wawili wangekimbizaje elfu kumi,
Kama Mwamba wao asingaliwauza,
Kama Bwana asingaliwatoa?
(K) Naua Mimi, nahuisha Mimi.
Maana siku ya msiba wao imekaribia,
Na mambo yatakayowapata yatafanya haraka.
Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake,
Atawahurumia watumwa wake.
(K) Naua Mimi, nahuisha Mimi.
Zab 25:4, 5
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako.
Aleluya.
Mt 19:23–30
Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno, wakisema, Ni nani basi awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana. Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi? Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele. Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.
Maoni
Ingia utoe maoni