Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 18 ya Mwaka (Jumapili, Agosti 04, 2024)  

Somo la 1

Kut 16:2-4, 12-15

Mkutano mzima wa wana wa Israeli uliwanung’unukia Musa na Haruni, huko barani; wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana ktika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote. Ndipo Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. Nimeyasikia manung’uniko ya wana wa Israeli; haya! Sema nao, ukinena, Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. Ikawa wakati wa jioni; kware wakakaribia, wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo. Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao Bwana amewapa ninyi, mle.

Wimbo wa Katikati

Zab 78:3-4, 23-25, 54

Mambo tuliyosikia na kuyafahamu,
Ambayo baba zetu walituambia.
Hayo hatutawaficha wana wao,
Huku tukiwaambia kizazi kingine,
Sifa za Bwana, na nguvu zake.
(K) Akawanyeshea mana ili wale; akawapa nafaka ya mbinguni.

Lakini aliyaamuru mawingu juu;
Akaifungua milango ya mbinguni;
Akawanyeshea mana ili wale;
Akawapa nafaka ya mbinguni.
(K) Akawanyeshea mana ili wale; akawapa nafaka ya mbinguni.

Mwanadamu akala chakula cha mashujaa;
Aliwaplekea chakula cha kuwashibisha.
Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu,
Mlima alionunua kwa mkono wake wa kuume.
(K) Akawanyeshea mana ili wale; akawapa nafaka ya mbinguni.

Somo la 2

Ef 4:17, 20-24

Nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waendavyo, katika ubatili wa nia zao. Basi ninyi, sivyo mlivyojifunza Kristo, ikiwa mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika Yesu, mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.

Shangilio

1Sam 3:9; Yn 6:68

Aleluya, aleluya,
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia; Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.

Injili

Yn 6:24-35

Mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu. Hata waliomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa? Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu. Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu. Mmwamini yeye aliyetumwa nay eye. Wakamwambia, unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani? Baba zetu waliila mana jangwani, kama vile ilivyoandikwa. Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale. Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa naye aniaminiye hataona kiu kamwe.

Maoni


Ingia utoe maoni