Masomo ya Misa
Jumanne ya 17 ya Mwaka (Jumanne, Julai 30, 2024)
Yer 14:17-22
Macho yangu na yatiririke machozi, usiku na mchana, wala yasikome; kwa maana bikira, binti ya watu wangu, amevunjika mavunjiko makuu, kwa jeraha isiyoponyeka. Nikitoka kwenda shambani, tazama, wako huko waliouawa kwa upanga! Na nikiingia mjini, tazama, wamo humo wanaougua kwa sababu ya njaa! Maana nabii na kuhani, wote wawili, huenda huko na huko katika nchi, wala hawana maarifa. Je! Umemkataa Yuda kabisa? Roho yako imeichukia Sayuni? Mbona umetupiga, tusiwe na dawa ya mema yoyote; tulitazamia wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu! Ee Bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi. Usituchukie, kwa ajili ya jina lako; usikifedheheshe kiti cha enzi cha utukufu wako; kumbuka, usilivunje agano ulilofanya nasi. Je! Katika vitu vya ubatili vya mataifa, kiko kiwezacho kuleta mvua? Je! Mbingu zaweza kutoa manyunyu! Je! Si wewe, Ee Bwana, Mungu wetu? Kwa sababu hiyo tutakungoja; kwa kuwa wewe umevifanya vitu hivi vyote.
Zab 79:8-9,11, 13
Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima.
Kwa maana tumedhilika sana.
(K) Kwa ajili ya utukufu wa jina lako, utusaidie, Ee Bwana.
Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie,
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utudhofiri dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako.
(K) Kwa ajili ya utukufu wa jina lako, utusaidie, Ee Bwana.
Kuugua kwake aliyefungwa na kuingia mbele zako,
Kwa kadiri ya uwezo wa mkono wako
Uwahifadhi wana wa mauti.
Na sisi tulio watu wako, na kondoo za malisho yako,
Tutakushukuru milele;
Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi.
(K) Kwa ajili ya utukufu wa jina lako, utusaidie, Ee Bwana.
Ebr 4:12
Aleluya, aleluya,
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu, li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya.
Mt 13:36–43
Yesu aliwaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie.
Maoni
Ingia utoe maoni