Masomo ya Misa
Jumatano ya 1 ya Majilio (Jumatano, Novemba 30, 2016)
Rum 10:9-18
Wapendwa ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
Zab 19:8, 9, 10, 11
Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.
(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.
Maagizo ya Bwana ni ya adili, Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi, Huyatia macho nuru.
(K)Sauti yao imeenea duniani mwote.
Kicho cha Bwana ni kitakatifu, Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli, Zina haki kabisa.
(K)Sauti yao imeenea duniani mwote.
Ni za kutamanika kuliko dhahabu, Kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali, Kuliko sega la asali.
(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.
Mt. 4:18
Aleluya, aleluya,
Bwana asema, Nifuateni, nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.
Aleluya.
Mt 4:18-22
Naye Yesu alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata.
Maoni
Ingia utoe maoni