Masomo ya Misa
Jumamosi ya 16 ya Mwaka (Jumamosi, Julai 27, 2024)
Yer 7:1–11
Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema, Simama langoni pa nyumba ya Bwana, ukatangaze hapo neno hili, ukisema, Sikilizeni neno la Bwana, ninyi nyote wa Yuda, mnaoingia katika malango haya ili kumwabudu Bwana. Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa. Msitumainie maneno ya uongo, mkisema, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana ndiyo haya. Maana kama mkitengeneza kabisa njia zenu na matendo yenu; kama mkihukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake; kama hamwonei mgeni wala yatima, wala mjane, wala kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, wala kuifuata miungu mingine kwa hasara yenu wenyewe; ndipo nitakapowakalisha mahali hapa, katika nchi hii niliyowapa baba zenu, tokea zamani hata milele. Angalieni, mnatumainia maneno ya uongo, yasiyoweza kufaidia. Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo na kumfukizia Baali uvumba, na kuifuata iungu mingine ambayo hamkuijua; kisha mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na kusema, Tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote? Je! Nyumba hii iitwayo kwa jina langu, imekuwa pango la wanyang’anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema Bwana.
Zab 84:2–5, 7, 10
Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana,
Naam na kuzikondea.
Moyo wangu na mwili wangu,
Vinamlilia Mungu aliye hai.
(K) Maskani zako zapendeza kama nini, ee Bwana wa majeshi.
Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kiota,
Alipoweka makinda yake.
Kwenye madhabahu zako, ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu.
(K) Maskani zako zapendeza kama nini, ee Bwana wa majeshi.
Heri wakaao nyumbani mwako
Wanakuhimidi damima.
Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
(K) Maskani zako zapendeza kama nini, ee Bwana wa majeshi.
Huendelea toka nguvu hata nguvu,
Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu.
Hakika siku moja katika nyua zako
Ni bora kuliko siku elfu.
Ningependa kuwa bawabu
Nyumbani mwa Mungu wangu,
Kuliko kukaa hema za uovu.
(K) Maskani zako zapendeza kama nini, ee Bwana wa majeshi.
Zab 119:105
Aleluya, aleluya,
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga katika njia yangu.
Aleluya.
Mt 13:24–30
Yesu aliwatolea makutano mfano akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala akaja adui yake akapanda magugu katikati ya agano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.
Maoni
Ingia utoe maoni