Ijumaa. 18 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 16 ya Mwaka (Ijumaa, Julai 26, 2024)  

Somo la 1

Yer 3:14–17

Rudini, enyi watoto wenye kuasi, asema Bwana; maana mimi ni mume wenu; nami nitatwaa mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja, nami nitawaleta hata Sayuni; nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu. Kisha itakuwa mtakapoongezeka na kuwa wengi katika nchi hiyo, asema Bwana, siku zile hawatasema tena, Sanduku la agano la Bwana; wala halitaingia moyoni; wala hayatafanyika hayo tena. Wakati ule watauita Yerusalemu kiti cha enzi cha Bwana; na mataifa yote watakusanyika huko Yerusalemu, kwa ajili ya jina la Bwana; wala hawatakwenda tena kwa ukaidi wa moyo wao mbaya.

Wimbo wa Katikati

Yer 31:10–13

Lisikieni neno la Bwana, enyi mataifa,
Litangazeni visiwani mbali,
Mkaseme: Aliyemtawanya Israeli atamkusanya,
Na kumlinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.
(K) Bwana anatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo,
Amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.
Nao watakuja na kuimba katika mlima Sayuni,
Wataukimbilia wema wa Bwana, nafaka, na divai,
Na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe.
(K) Bwana anatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,
Na vijana na wazee pamoja,
Maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,
Nami nitawafariji
Na kuwafurahisha waache huzuni yao.
(K) Bwana anatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Shangilio

Mt 11:25

Aleluya, aleluya,
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.

Injili

Mt 13:18–23

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi. Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia. Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa, naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai. Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini.

Maoni


Ingia utoe maoni