Jumapili. 08 Septemba. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuu ya Mt. Maria Magdalena (Jumatatu, Julai 22, 2024)  

Somo la 1

Wim 3:1-4

Usiku kitandani nalimtafuta mpendwa wa nafsi yangu, Nalimtafuta, nisimpate. Nikasema, Haya, niondoke nizunguke mjini, Katika njia zake na viwanjani, Nimtafute mpendwa wa nafsi yangu. Nikamtafuta, nisimpate. Walinzi wazungukao mjini waliniona; Je! mmemwona mpendwa wa nafsi yangu? Kitambo kidogo tu nikiisha kuwaondokea, Nikamwona mpendwa wa nafsi yangu.

Wimbo wa Katikati

Zab 63: 1-5, 7-8

Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema,
Nafsi yangu inakuonea kiu,
Mwili wangu wakuonea shauku,
Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.
(K) Nafsi yangu inakuonea kiu, Ee Bwana.

Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu,
Nizione nguvu zako na utukufu wako.
Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai;
Midomo yangu itakusifu.
(K) Nafsi yangu inakuonea kiu, Ee Bwana.

Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai;
Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono;
Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha.
(K) Nafsi yangu inakuonea kiu, Ee Bwana.

Maana Wewe umekuwa msaada wangu,
Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.
Nafsi yangu inakuandama sana;
Mkono wako wa kuume unanitegemeza.
(K) Nafsi yangu inakuonea kiu, Ee Bwana.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Maria tuambie: sema uliyoona njiani. Kaburi lilimfadhi yule aliye Mzima; Niliona utukufu wa Kristu alipokuwa akifufuka.
Aleluya.

Injili

Yn 20:1-2, 11-18

Siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalena alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka. Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, Mama unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa. Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (yaani, Mwalimu wangu). Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo.

Maoni

Kepha Maswaga

Napenda katoliki

Kepha Maswaga

Yesu

Ingia utoe maoni