Masomo ya Misa
Jumatano ya 15 ya Mwaka (Jumatano, Julai 17, 2024)
Isa 10:5–7, 13–16
Bwana asema hivi: Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu! Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani. Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache. Kwa maana amesema, Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; name nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa. Na mkono wangu umezitoa maji za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia. Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti. Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, atawapekelea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto.
Zab 94:5–10, 14–15
Ee Bwana, wanawaseta watu wako;
Wanauseta urithi wako;
Wanamwua mjane na mgeni;
Wanawafisha yatima.
(K) Bwana hatawatupa watu wake.
Nao husema, Bwana haoni;
Mungu wa Yakobo hafikiri.
Enyi wajinga miongoni mwa watu fikirini;
Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili?
(K) Bwana hatawatupa watu wake.
Aliyelitia sikio mahali pake asisikie?
Aliyelifanya jicho asilione?
Awaadhibuye mataifa asikemee?
Amfundishaye mwanadamu asijue?
(K) Bwana hatawatupa watu wake.
Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake.
Wala hutauacha urithi wake,
Maana hukumu itairejea haki,
Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata.
(K) Bwana hatawatupa watu wake.
Zab 27:11
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unifundishe njia yako, na kuniongoza katika njia iliyonyoka.
Aleluya.
Mt 11:25–27
Wakati ule Yesu alijibu akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yenyote ambaye Mwana apenda kumfunulia.
Maoni
Ingia utoe maoni