Jumanne. 22 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 14 ya Mwaka (Jumatatu, Julai 08, 2024)  

Somo la 1

Hos 2:14–16, 19–20

Bwana asema hivi: Angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na kusema naye maneno ya kumtuliza moyo. Naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri. Tena siku hiyo itakuwa, asema Bwana, utaniita Ishi, wala hutaniita tena, Baali. Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema. Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua Bwana.

Wimbo wa Katikati

Zab 145:2–9

Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.
Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana,
Wala ukuu wake hautambulikani.
(K) Bwana ana fadhili ni mwingi wa huruma.

Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako,
Kitayatangaza matendo yako makuu.
Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako,
Na matendo yako yote ya ajabu.
(K) Bwana ana fadhili ni mwingi wa huruma.

Watu watayataja matendo yako ya kutisha,
Name nitausimulia ukuu wako.
Watalihubiri kumbukumbu la wema wako mkuu,
Wataiimba haki yako.
(K) Bwana ana fadhili ni mwingi wa huruma.

Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi kwa hasira, ni mwingi wa rehema.
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
(K) Bwana ana fadhili ni mwingi wa huruma.

Shangilio

Yn 8:12

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya.

Injili

Mt 9:18–26

Yesu alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu, Imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote.

Maoni


Ingia utoe maoni