Jumanne. 16 Julai. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 13 ya Mwaka (Jumamosi, Julai 06, 2024)  

Somo la 1

Amo 9:11–15

Bwana asema hivi: Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale; wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema Bwana, afanyaye hayo. Angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo huyo alimaye atamfikilia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka. Nami nitawarejeza tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watafanyiza bustani, na kula matunda yake. Nami nitawapanda katika nchi yao, wala hawatang’olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa, asema Bwana, Mungu wako.

Wimbo wa Katikati

Zab 85:8, 10–13

Nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
maana atawaambia watu wake amani.
Naam, na watauwa wake pia.
Bali wasiurudie upumbavu tena.
(K) Bwana anawaambia watu wake amani.

Fadhili na kweli zimekutana,
haki na amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
haki imechungulia kutoka mbinguni.
(K) Bwana anawaambia watu wake amani.

Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
na nchi itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.
(K) Bwana anawaambia watu wake amani.

Shangilio

Mt 11:25

Aleluya, aleluya,
Nashukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.

Injili

Mt 9:14–17

Wanafunzi wake Yohane walimwendea Yesu wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga. Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote.

Maoni


Ingia utoe maoni