Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumapili ya 1 ya Majilio (Jumapili, Novemba 27, 2016)  

Somo la 1

Isa 2:1-5

Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amozi katika habari za Yuda na Yerusalemu. Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya Bwana.

Wimbo wa Katikati

Zab 122:1-4, 8-9

Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.
(K) Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana.

Ee Yerusalemu uliyejengwa Kama mji ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila, Kabila za Bwana;
(K) Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana.

Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu Niseme sasa, Amani ikae nawe.
Kwa ajili ya nyumba ya Bwana, Mungu wetu, Nikutafutie mema.
(K) Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana.

Somo la 2

Rum 13:11-14

Ndugu zangu, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru.Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.

Shangilio

Zab 85:7

Aleluya, aleluya
Ee Bwana utuonyesha rehema zako, Utupe na wokovu wako,
Aleluya

Injili

Mt 24:37-44

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.

Maoni


Ingia utoe maoni