Masomo ya Misa
DOMINIKA, JUMA LA 2 LA KWARESIMA (Jumapili, Februari 21, 2016)
Mwa. 15:5-12, 17-18
Mungu akamleta Ibrahimu nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. Kisha akamwambia, Mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi. Akasema, Ee Bwana Mungu, nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati.
Zab. 27:1,7-9, 13-14 (K) 1
Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Ee Bwana, usikie kwa sauti yangu ninalia,
Unifadhili, unijibu.
Moyo wangu umekuambia,
Bwana uso wako nitautafuta.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Usinifiche uso wako,
Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
Umekuwa msaada wangu, usinitupe,
Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Flp. 3:17-4:1
Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi. Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo; mwisho wao ni uharibifu, mungu wao nit umbo. Utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani. Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake. Basi ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji yangu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu.
Lk. 9:28b-36
Yesu aliwatwaa Petro na Yohane na Yakobo akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kuomba kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walioonekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu. Petro na wale waliokuwa pamoja na walikuwa wameelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka walikuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye. Ikawa hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro akimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo. Alipokuwa akisema hayo lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo. Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye. Na sauti hiyo ilipokwisha, Yesu alionekana yup eke yake. Nao wakanyamaza, wasitangaze kwa mtu siku zile lolote katika hayo waliyoyaona.
Maoni
Ingia utoe maoni