Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 12 ya Mwaka (Jumanne, Juni 25, 2024)  

Somo la 1

2Fal 19:9-11, 14-21, 31-36

Na aliposikia habari ya Tirhaka mfalme wa Kushi, ya kwamba, Tazama, ametoka ili kupigana nawe; alituma wajumbe kwa Hezekia mara ya pili, kusema, Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru. Tazama, umesikia ni mambo gani wafalme wa Ashuru waliyozitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa; je! Utaokoka wewe?Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya Bwana, akaukunjua mbele za Bwana. Naye Hezekia akaomba mbele za Bwana, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, Ee Bwana, usikie; fumbua macho yako, Ee Bwana, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, Bwana, wafalme wa Ashuru wamewaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo sababu wakaiharibu. Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe Bwana Mungu, wewe peke yako. Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akisema, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru, mimi nimekusikia. Tamko alilolitamka Bwana katika habari zake ndilo hili, Bikira, binti Sayuni, amekudharau, na kukudhihaki sana; binti Yerusalemu ametikisa kichwa chake juu yako.Maana mabaki yatatoka katika Yerusalemu, na wao watakaookoka katika mlima wa Sayuni wivu wa Bwana utatimiza jambo hilo. Basi Bwana asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hatauingia mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake. Njia ile ile aliyojia, kwa njia iyo hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu, asema Bwana. Maana nitaulinda mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu. Ikawa usiku uo huo malaika wa Bwana alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na themanini na tano elfu. Na watu walipoondoka asubuhi na mapema, kumbe! Hao walikuwa maiti wote pia. Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda zake, akarudi akakaa Ninawi.

Wimbo wa Katikati

Zab 48:1-3, 9-10

Bwana ndiye aliye mkuu, Na mwenye kusifiwa sana.
Katika mji wa Mungu wetu, Katika mlima wake mtakatifu.
Kuinuka kwake ni mzuri sana, Ni furaha ya dunia yote.
(K) Mji wa Mungu wetu; Mungu ataufanya imara hata milele.

Mlima Sayuni pande za kaskazini, Mji wa Mfalme mkuu.
Mungu katika majumba yake Amejijulisha kuwa ngome.
(K) Mji wa Mungu wetu; Mungu ataufanya imara hata milele.

Tumezitafakari fadhili zako, Ee Mungu, Katikati ya hekalu lako.
Kama lilivyo jina lako, Ee Mungu,
Ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia.
Mkono wako wa kuume umejaa haki;
(K) Mji wa Mungu wetu; Mungu ataufanya imara hata milele.

Shangilio

Yn 8:12

Aleluya, aleluya
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya

Injili

Mt 7:6, 12-14

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua. Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii. Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.

Maoni


Ingia utoe maoni