Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 34 ya Mwaka (Jumamosi, Novemba 26, 2016)  

Somo la 1

Ufu 22:1-7

Malaika alinionyesha, mimi Yohane, mto wa maji ya uzima, wenye kung'aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo, katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa. Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia; nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao. Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele. Kisha akaniambia, Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi. Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.

Wimbo wa Katikati

Zab 95:1-7

Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi.
(K) Maranatha, Uje Bwana Yesu.

Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,
Na Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Mkononi mwake zimo bonde za dunia,
Hata vilele vya milima ni vyake.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya,
Na mikono yake iliumba nchi kavu.
(K) Maranatha, Uje Bwana Yesu.

Njoni, tuabudu, tusujudu, Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu, Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
(K) Maranatha, Uje Bwana Yesu.

Shangilio

Zab. 119:135

Aleluya, aleluya,
Umwangazie mtumishi wako uso wako, na kunifundisha amri zako.
Aleluya.

Injili

Lk 21:34-36

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima. Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.

Maoni


Ingia utoe maoni