Jumamosi. 27 Julai. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Mt. Barnaba, Mtume. (Jumanne, Juni 11, 2024)  

Somo la 1

Mdo 11:21-26, 13:1-3

Watu wengi waliamini, wakamwelekea Bwana. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Baranaba, aende hata Antiokia. Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote wawaambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na Imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. Kasha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia. Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.

Wimbo wa Katikati

Zab 98:1-6

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa.

Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa.

Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa.

Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu.
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri kuwa Bwana. Jamii tukufu ya mitume inakusifu.
Aleluya.

Injili

Mt 5:13-16

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

Maoni


Ingia utoe maoni