Ijumaa. 21 Juni. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 10 ya Mwaka (Jumatatu, Juni 10, 2024)  

Somo la 1

1Fal 17:1-6

Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu. Neno la Bwana likamjia, kusema, Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani. Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko. Basi akaenda akafanya kama alivyosema Bwana; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerithi, kinachokabili Yordani. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.

Wimbo wa Katikati

Zab 121:1-8

Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi?
Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.
(K) Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.

Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye;
Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.
(K) Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.

Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume.
Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku.
(K) Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.

Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako.
Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.
(K) Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.

Shangilio

Mt 5:12a

Aleluya, aleluya
Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni;
Aleluya

Injili

Mt 5:1-12

Naye Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.

Maoni


Ingia utoe maoni