Ijumaa. 21 Juni. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 10 ya Mwaka (Jumapili, Juni 09, 2024)  

Somo la 1

Mwa. 3:9-15

Bwana Mungu alimwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, naliogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.

Wimbo wa Katikati

Zab. 130

Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia,
Bwana, uisikie sauti yangu,
Masikio yako na yaisikilize
Sauti ya dua zangu.
(K) Maana kwa Bwana kuna fadhili, na kwake kuna ukombozi mwingi.

Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
Ee Bwana, nani angesimama?
Lakini kwako kuna msamaha,
Ili Wewe uogopwe.
(K) Maana kwa Bwana kuna fadhili, na kwake kuna ukombozi mwingi.

Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja,
Na neno lake nimelitumainia.
Nafsi yangu inamngoja Bwana,
Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi.
(K) Maana kwa Bwana kuna fadhili, na kwake kuna ukombozi mwingi.

Ee Israeli, umtarajie Bwana;
Maana kwa Bwana kuna fadhili,
Na kwake kuna ukombozi mwingi.
Yeye atamkomboa Israeli na maovu yake yote.
(K) Maana kwa Bwana kuna fadhili, na kwake kuna ukombozi mwingi.

Somo la 2

2Kor. 4:13-5:1

Kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama ilivyoandikwa, Naliamini na kwa sababu hiyo nalinena, sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena; tukijua ya kwamba yeye aliyefufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi. Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yetu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wan je unachakaa; lakni utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele. Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jingo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni.

Shangilio

Lk. 4:18-19

Aleluya, aleluya,
Bwana amenituma kuwahubiri maskini habari njema, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao.
Aleluya.

Injili

Mk. 3:20-35

Mkutano walikusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate. Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili. Nao waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo. Akawaita, akawaambia kwa mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani? Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama; na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama. Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo. Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake. Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele; kwa vile walivyosema, Ana pepo mchafu. Wakaja mamaye na nduguze, wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita. Na makutano walikuwa wameketi, wakimzunguka; wakamwambia, TAzama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta. Akawajibu, akisema, Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani? Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana mtu yeyote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.

Maoni


Ingia utoe maoni