Masomo ya Misa
Moyo Safi wa Bikira Maria Imakulata (Jumamosi, Juni 08, 2024)
2 Tim 4:1-8
Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake; lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo. Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako. Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.
Zab 71:8-9, 14-17, 22
Kinywa changu kitajazwa sifa zako, Na heshima yako mchana kutwa.
Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo usiniache.
(K)Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa.
Nami nitatumaini daima, Nitazidi kuongeza sifa zake zote.
Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa;
(K)Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa.
Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana MUNGU; Nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo.
(K)Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa.
Nami nitakushukuru kwa kinanda, Na kweli yako, Ee Mungu wangu.
Nitakuimbia Wewe kwa kinubi, Ee Mtakatifu wa Israeli.
(K)Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa.
Lk 2:19
Aleluya, aleluya
Abarikiwe Bikira Mariamu aliyeyaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.
Aleluya
Lk 2: 41-51
Wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.
Maoni
Ingia utoe maoni