Masomo ya Misa
Alhamisi ya 9 ya Mwaka (Alhamisi, Juni 06, 2024)
2Tim 2:8-15
Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao. Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.
Zab 25:4-5, 8-10, 14;
Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.
(K) Ee Bwana, unijulishe njia zako.
Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu,
Nakungoja Wewe mchana kutwa.
Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake.
(K) Ee Bwana, unijulishe njia zako.
Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli,
Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
Siri ya Bwana iko kwao wamchao,
Naye atawajulisha agano lake.
(K) Ee Bwana, unijulishe njia zako.
Yn 8:12
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema, Bwana, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya.
Mk 12:28-34
Mmoja wa waandishi alifika kwa Yesu akamwuliza, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza? Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja. nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi. Yule mwandishi akamwambia, Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia. Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo.
Maoni
Ingia utoe maoni