Masomo ya Misa
Jumanne ya 9 ya Mwaka (Jumanne, Juni 04, 2024)
2Pet 3:11-15, 17-18
Kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? Lakini, kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake. Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake. Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa. Basi, wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu, msije mkachukuliwa na kosa la hao wahalifu, mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu. Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele. Amina.
Zab 90:2-4,10,16
Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia,
Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi.
Wamrudisha mtu mavumbini,
Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kesha la usiku.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi.
Siku za miaka yetu ni miaka sabini,
Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini;
Na kiburi chake ni taabu na ubatili,
Maana chapita upesi tukatokomea mara.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi.
Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote
Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako,
Na adhama yako kwa watoto wao.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi.
Mt 4:4
Aleluya.
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Aleluya.
Mk 12:13-17
Walituma kwa Yesu baadhi ya Mafarisayo na Maherodi, ili wamnase kwa maneno. Hata walipofika walimwambia, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, wala hujali cheo cha mtu; kwa maana hutazami sura za watu; lakini katika kweli waifundisha njia ya Mungu. Je! Ni halali kumpa Kaisari kodi au siyo? Tumpe, tusimpe? Naye, akijua unafiki wao, akawaambia, Mbona mmejijaribu? Nileteeni dinari niione. Wakaileta. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Yesu akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu. Wakamstaajabia sana.
Maoni
Ingia utoe maoni