Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 7 ya mwaka (Alhamisi, Mei 23, 2024)  

Somo la 1

Yak 5:1-6

Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi.

Wimbo wa Katikati

Zab 49:13-19

Hiyo ndiyo njia yao, ujinga wao, Nao walioko baada yao huyaridhia maneno yao.
Kama kondoo wamewekwa kwenda kuzimu, Na mauti itawachunga;
(K)Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao

Watu wanyofu watawamiliki asubuhi; Umbo lao litachakaa, kao lao ni kuzimu.
Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, Atanitoa mkononi mwa kuzimu, maana atanikaribisha.
(K)Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao

Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi.
Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata.
(K)Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao

Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai, Na watu watakusifu ukijitendea mema,
Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake Hawataona nuru hata milele.
(K)Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao

Shangilio

1 The 2:13

Aleluya, aleluya
Mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli;
Aleluya

Injili

Mk 9:41-50

Yesu akawaambia wanafunzi wake, Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake. Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini. Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto. Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi.

Maoni

Martin Muteti

Atukunzwe MUNGU BABA MUNGU MWANA NA MUNGU ROHO MTAKATIFU

Ingia utoe maoni