Jumapili. 08 Septemba. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuu ya Mt. Matia Mtume (Jumanne, Mei 14, 2024)  

Somo la 1

Mdo 1:15-17, 20-26

Siku zile Petro alisimama kati ya ndugu zake (jumala ya majina ilipata mia na ishirini), akasema, Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi. katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu, kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii. Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi, Kikao chake na kiwe ukiwa, Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo; tena, Usimamizi wake autwae mwingine. Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohane, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi. Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe. Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.

Wimbo wa Katikati

Zab 113:1-8

Aleluya.
Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
Lisifuni jina la Bwana.
Jina la Bwana lihimidiwe
Tangu leo na hata milele.
(K) Amketishe pamoja na wakuu, pamoja na wakuu wa watu wake.

Toka maawio ya jua hata machweo yake
Jina la Bwana husifiwa.
Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote,
Na utukufu wake ni juu ya mbingu.
(K) Amketishe pamoja na wakuu, pamoja na wakuu wa watu wake.

Ni nani aliye mfano wa Bwana,
Mungu wetu aketiye juu;
Anyenyekeaye kutazama,
Mbinguni na duniani?
(K) Amketishe pamoja na wakuu, pamoja na wakuu wa watu wake.

Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Na kumpandisha maskini kutoka jaani.
Amketishe pamoja na wakuu,
Pamoja na wakuu wa watu wake.
(K) Amketishe pamoja na wakuu, pamoja na wakuu wa watu wake.

Shangilio

Yn 15:16

Aleluya, aleluya,
Ni mimi niliyewachagua ninyi, nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kukaa.
Aleluya.

Injili

Yn 15:9-17

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe. Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.

Maoni


Ingia utoe maoni