Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 7 ya Pasaka (Jumapili, Mei 12, 2024)  

Somo la 1

Mdo. 1 :15-17, 20a, 20c-26

Siku zile, alisimama Petro kati ya hao ndugu (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), akasema, Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu, kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii. Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi, Usimamizi wake autwae mwingine. Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohane, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi. Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe. Wakawapigia kura; kura ikamwa- ngukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.

Wimbo wa Katikati

Zab. 103 :1-2, 11-12, 19-20

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni,
Au: Aleluya.

Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
(K) Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni,
Au: Aleluya.

Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni,
Na ufalme wake unavitawala vitu vyote.
Mhimidini Bwana, enyi malaika zake,
Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake.
(K) Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni,
Au: Aleluya.

Somo la 2

1 Yoh. 4 :11-16

Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu. Katika hili tunafahamu ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametushirikisha Roho wake. Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu, Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kweti sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaayt katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungi hukaa ndani yake.

Shangilio

Yn 14:18

Aleluya, aleluya.
Sitawaacha ninyi yatima, asema Bwana; naja kwenu, na mioyo zenu zitajaa na furaha.
Aleluya.

Injili

Yn 17: 11b-19

Siku ile, Yesu aliinua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, iliandiko litimie. Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.

Maoni


Ingia utoe maoni