Masomo ya Misa
Jumamosi ya 6 ya Pasaka (Jumamosi, Mei 11, 2024)
Mdo 18:23-28
Paulo, akiisha kukaa Antiokia siku kadha wa kadha aliondoka, akapita kati ya nchi ya Galatia na Frigia, mji kwa mji, akiwathibitisha wanafunzi. Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzaliwa wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohane tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe; naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.
Zab 47: 1-2, 7-9
Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe,
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au: Aleluya.
Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili.
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu.
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au: Aleluya.
Wakuu wa watu wamekusanyika,
Wawe watu wa Mungu wa Ibrahimu.
Maana ngao za dunia zina Mungu,
Ametukuka sana.
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au: Aleluya.
Yn 10:27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.
Yn 16:23-28
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu. Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa yaja ambayo sitasema nanyi tena kwa mithali; lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba. Na siku ile mtaomba kwa jina langu; wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba. Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.
Maoni
Ingia utoe maoni