Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

KUTOLEWA BIKIRA MARIA HEKALUNI (Jumatatu, Novemba 21, 2016)  

Somo la 1

Zek. 2:10 – 13

Imba, furahi, Ee binti Sayuni; maana, tazama, anakuja, nami nitakaa, kati yako, asema Bwana. Na mataifa mengi watajiunga na Bwana katika siku ile, nao watakuwa watu wangu; nami nitakaa kati yako, nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwako. Na Bwana atairithi Yuda, iwe sehemu yake katika nchi takatifu, naye atachagua Yerusalemu tena. Nyamazeni, ninyi nyote wenye mwili, mbele za Bwana; kwa maana ameamka, na kutoka katika maskani yake takatifu.

Wimbo wa Katikati

Lk. 1:46 – 55

Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu.
(K) Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.

Kwa kuwa ameutazama
Unyonge wa mjakazi wake.
Kwa maana, tazama, tokea sasa
Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;
Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu,
Na jina lake ni takatifu.
(K) Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.

Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi
Kwa hao wanaomcha.
Amefanya nguvu kwa mkono wake;
Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao.
(K) Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.

Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi;
Na wanyonge amewakweza.
Wenye njaa amewashibisha mema,
Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu.
(K) Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.

Amemsaidia Israeli, mtumishi wake;
Ili kukumbuka rehema zake;
Kama alivyowaambia baba zetu,
Ibrahimu na uzao wake hata milele.
(K) Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.

Shangilio

Lk. 1:28

Aleluya, aleluya,
Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa katika wanawake.
Aleluya.

Injili

Lk. 11:27 – 28

Yesu aliposema maneno hayo, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, Heri tumbo lililokuzaa, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.

Maoni


Ingia utoe maoni