Masomo ya Misa
Dominika ya 5 ya Pasaka (Jumapili, Aprili 28, 2024)
Mdo 9:26-31
Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao wakajaribu kumwua. Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakampeleka aende Tarso. Basi kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu.
Zab 22:25-27, 28-31
Kwako zinatoka sifa zangu Katika kusanyiko kubwa.
Nitaziondoa nadhiri zangu Mbele yao wamchao.
Wapole watakula na kushiba,
Wamtafutao Bwana watamsifu;
Mioyo yenu na iishi milele.
(K) Kwako, Bwana, zinatoka sifa zangu katika kusanyiko kubwa.
Miisho yote ya dunia itakumbuka,
Na watu watamrejea Bwana;
Jamaa zote za mataifa watamsujudia.
Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu,
Humwinamia wote washukao mavumbini;
(K) Kwako, Bwana, zinatoka sifa zangu katika kusanyiko kubwa.
Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,
Wazao wake watamtumikia.
Zitasimuliwa habari za Bwana,
Kwa kizazi kitakachokuja,
Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake,
Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.
(K) Kwako, Bwana, zinatoka sifa zangu katika kusanyiko kubwa.
1 Yoh 3:18-24
Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake, ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote. Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa.
Yn 15:4-5
Aleluya, aleluya
Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu, akaaye ndani yangu, huyo huzaa sana
Aleluya.
Yn 15:1-8
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.
Maoni
Ingia utoe maoni