Jumatatu. 06 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 4 ya Pasaka (Jumatatu, Aprili 22, 2024)  

Somo la 1

Mdo 11:1-18

Siku zile, mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu. Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye, wakisema, uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao. Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema, Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikia. Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wan chi wenye miguu mine, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani. Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule. Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu. Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni. Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria. Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishwi. Ndugu hawa sita nao wakaenda nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule; akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro, atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote. Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukuia kama alivyotushukia sisi mwanzo. Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohane alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatiza kwa Roho Mtakatifu. Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu? Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba lilitalo uzima.

Wimbo wa Katikati

Zab 42:1-2, 43:2-3

Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji,
Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, ee Mungu.
(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.

Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,
Lini nitakapoikuja nionekane mbele za Mungu?
(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.

Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze,
Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu na hata maskani yako.
(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.

Hivyo nitakwenda madhabahuni mwa Mungu,
Kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu;
Nitakusifu kwa kinubi, ee Mungu, Mungu wangu.
(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.

Shangilio

Ufu 1:5

Aleluya, aleluya,
Ee Kristo, yu shahidi aliye mwaminifu mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia.
Aleluya.

Injili

Yn 10:11-18

Yesu alisema: Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.

Maoni


Ingia utoe maoni