Masomo ya Misa
Dominika ya 4 ya Pasaka (Jumapili, Aprili 21, 2024)
Mdo.4:8-12
Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.
Zab 118:1,8-9,21-23,26,28-29
Aleluya.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Ni heri kumkimbilia Bwana
Kuliko kuwatumainia wanadamu.
Ni heri kumkimbilia BWANA.
Kuliko kuwatumainia wakuu.
(K)Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni
Nitakushukuru kwa maana umenijibu, Nawe umekuwa wokovu wangu.
Jiwe walilolikataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu.
(K)Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni
Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana;
Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana
Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru,
Ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza.
Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
(K)Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni
1Yoh.3:1-2
Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.
Yn 10:14
Aleluya aleluya
Mimi ndimi mchungaji mwema;
nao walio wangu nawajua;
Nao walio wangu wanijua mimi .
Aleluya
Yn.10:11-18
Siku ile,Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.
Maoni
Ingia utoe maoni