Masomo ya Misa
Jumamosi ya 2 ya Pasaka (Jumamosi, Aprili 13, 2024)
Mdo 6:1-7
Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno. Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao. Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani.
Zab 33:1-2, 4-5, 18-19
Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
(K)Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.
Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana.
(K)Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.
Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa.
(K)Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.
Yn. 10:27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.
Yn 6:16-21
Hata ilipokuwa jioni wanafunzi wake wakatelemka baharini wakapanda chomboni, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu. Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa. Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope. Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia nchi waliyokuwa wakiiendea.
Maoni
Ingia utoe maoni