Jumatatu. 06 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 2 ya Pasaka (Alhamisi, Aprili 11, 2024)  

Somo la 1

Mdo 5:27-33

Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio. Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua.

Wimbo wa Katikati

Zab 34:1, 8, 15-19

Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
Heri mtu yule anayemtumaini.
(K)Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.

Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,
Na masikio yake hukielekea kilio chao.
Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote.
(K)Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.

Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Mateso ya mwenye haki ni mengi,
Lakini Bwana humponya nayo yote.
(K)Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.

Shangilio

Yn 20:29

Aleluya, aleluya,
Umesadiki, Toma, kwa kuwa umeniona, wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Aleluya.

Injili

Yn 3:31-36

Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote. Yale aliyoyaona na kuyasikia ndiyo anayoyashuhudia, wala hakuna anayeukubali ushuhuda wake. Yeye aliyeukubali ushuhuda wake ametia muhuri ya kwamba Mungu ni kweli. Kwa kuwa yeye aliyetumwa na Mungu huyanena maneno ya Mungu; kwa sababu hamtoi Roho kwa kipimo. Baba ampenda Mwana, naye amempa vyote mkononi mwake. Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.

Maoni

Martin Muteti

Atukunzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu kama mwanzo na siku zote milele na milele amina

Ingia utoe maoni