Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya Oktava ya Pasaka (Jumamosi, Aprili 06, 2024)  

Somo la 1

Mdo 4:13–21

Siku ile, makuhani na akida wa hekalu walipoona ujasiri wa Petro na Yohane, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu. Na wakimwona yule aliyeponywa akisimama pamoja nao hawakuwa na neno la kujibu. Wakawaamuru kutoka katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao, wakisema, Tuwafanyieni watu hyawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana. Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili. Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. Petro na Yohane wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia. Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka.

Wimbo wa Katikati

Zab 118:1, 14–21

Aleluya,
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu,
Naye amekuwa wokovu wangu.
Sauti ya furaha na wokovu,
Imo hemani mwao wenye haki.
(K) Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.

Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Sitakufa bali nitaishi,
Nami nitayasimulia matendo ya Bwana.
Bwana ameniadhibu sana,
Lakini hakuniacha nife.
(K) Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.

Nifungulieni malango ya haki,
Nitaingia na kumshukuru Bwana.
Lango hili ni la Bwana,
Wenye haki ndio watakaoliingia.
Nitakushukuru kwa maana umenijibu,
Nawe umekuwa wokovu wangu.
(K) Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.

Shangilio

Zab 118:24

Aleluya, aleluya,
Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutaishangilia na kuifurahia.
Aleluya.

Injili

Mk 16:9–15

Yesu alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba. Huyo akashika njia akawapasha habari wale waliokuwa pamoja naye, nao wakali wanaomboleza na kulia. Walakini hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki. Baada ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine; nao walikuwa wakishika njia kwenda shamba. Na hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwasadiki. Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu. Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

Maoni


Ingia utoe maoni