Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 33 ya Mwaka (Ijumaa, Novemba 18, 2016)  

Somo la 1

Mdo 28:11-16, 30-31

Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha. Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu. Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli. Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi tukafika Rumi. Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka. Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda.Akakaa muda wa miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.

Wimbo wa Katikati

Zab 98:1-6

Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe, Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
(K) Bwana ameidhihirisha haki yake machoni pa mataifa.

Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K) Bwana ameidhihirisha haki yake machoni pa mataifa.

Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu.
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.
(K) Bwana ameidhihirisha haki yake machoni pa mataifa.

Shangilio

2Kor. 5:19

Aleluya, aleluya,
Mungu alikuwa ndani ya Kristu, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya.

Injili

Mt 14:22-33

Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.

Maoni


Ingia utoe maoni