Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 5 ya Kwaresima (Jumamosi, Machi 23, 2024)  

Somo la 1

Eze 37:21–28

Bwana Mungu asema hivi: Tazama, nitawatwaa wana wa Israeli toka kati ya mataifa walikokwenda, nami nitawakusanya pande zote, na kuwaleta katika nchi yao wenyewe; nami nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi hiyo, juu ya milima ya Israeli; na mfalme mmoja atakuwa mfalme wao wote; wala hawatakuwa tena mataifa mawili, wala hawatagawanyikana kuwa falme mbili tena, hata milele. Wala hawatajitia uchafu tena kwa vinyago vyao, wala kwa vitu vyao vichukizavyo, wala kwa makosa yao mmojawapo; lakini nitawaokoa, na kuwatoa katika makao yao yote, ambayo wamefanya dhambi ndani yake, nami nitawatakasa; basi watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja; nao wataenenda katika hukumu zangu, na kuzishika amri zangu, na kuzitenda. Nao watakaa katika nchi niliyompa Yakobo, mtumishi wangu, walimokaa baba zenu; nao watakaa humo, wao na watoto wao, na watoto wa watoto wao, milele; na Daudi, mtumishi wangu, atakuwa mkuu wao milele. Tena nitafanya agano la Amani pamoja nao; litakuwa agano la milele pamoja nao; naami nitaweka na kuwazidisha, na patakatifu pangu nitapaweka katikati yao milele. Tena maskani yangu itakuwa pamoja nao; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Na mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, mimi niwatakasaye Israeli, patakatifu pangu patakapokuwa katikati yao milele.

Wimbo wa Katikati

Yer 31:10–13

Lisikieni neno la Bwana, enyi mataifa,
Litangazeni visiwani mbali;
Mkaseme: Aliyemtawanya Israeli atamkusanya,
Na kumlinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.
Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo,
Amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.
(K) Bwana anatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Watakuja na kuimba katika mlima Sayuni.
Wataukimbilia wema wa Bwana,
Nafaka, na divai, na mafuta,
Na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe.
(K) Bwana anatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,
Na vijana na wazee pamoja;
Maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,
Nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao.
(K) Bwana anatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Shangilio

Zab 95:8 , 9

Leo msifanye migumu mioyo yenu, lakini msikie sauti yake Bwana.

Injili

Yn 11:45–57

Wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Maria, na kuyaona yale aliyoyafanya Yesu, wakamwamini. Lakini wengine wakaenda zao kwa Mafarisayo, wakawaambia aliyoyafanya. Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi. Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja watamuondolea mahali petu na taifa letu. Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui neno lolote; wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima. Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa hilo, wala si kwa ajili ya taifa hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili waawe wamoja. Basi tangu siku ile walifanya shauri la kumwua. Kwa hiyo Yesu hakutembea tena kwa wazi katikati ya Wayahudi; bali alitoka huko, akaenda mahali karibu na jangwa, mpaka mji uitwao Efraimu; akakaa huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; na wengi wakakwea toka mashambani kwenda Yerusalemu kabla ya Pasaka, ili wajitakase. Basi wao wakamtafuta Yesu, wakasemezana hali wamesimama hekaluni, Mwaonaje? Haji kabisa sikukuu hii? Na wakuu wa makuhani wa Mafarisayo walikuwa wametoa amri ya kwamba mtu akijua alipo, alete habari, ili wapate kumkamata.

Maoni


Ingia utoe maoni