Ijumaa. 03 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 5 ya Kwaresima (Jumapili, Machi 17, 2024)  

Somo la 1

Yer 31:31-34

Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana. Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.

Wimbo wa Katikati

Zab 51:1-2, 10-13

Ee Mungu, unirehemu,
Sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu.
(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.

Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.
(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.

Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
Nitawafundisha wakosaji njia zako,
Na wenye dhambi watarejea kwako.
(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.

Somo la 2

Ebr 5:7-9

Yesu, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii;

Shangilio

Yn 12:26

Mtu akinitumikia, na anifuate, asema Bwana; Nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo.

Injili

Yn 12:20-33

Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu. Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu. Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu. Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu. Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena. Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye. Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu. Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu. Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa.

Maoni


Ingia utoe maoni