Masomo ya Misa
Jumatano ya 4 ya Kwaresima (Jumatano, Machi 13, 2024)
Isa 49:8-15
Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza. Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia kuu zangu zitatukuzwa zote. Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya sinimu. Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, naye atawahurumia watu wake walioteswa. Bali Sayuni alisema, Yehova ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.
Zab 145:8-9, 13-14, 17-18
Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
(K) Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma.
Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Ni mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinama chini.
(K) Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma.
Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu.
(K) Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma.
Mt 4:4
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Yn 5:17-30
Yesu aliwajibu Wayahudi: Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. Basi kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu. Basi Yesu akajibu, akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile. Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizi atamwonyesha ili ninyi mpate kustaajabu. Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana ahuisha wale awatakao. Tena Baba hamhukumu mtu yeyote, bali amempa Mwana hukumu yote, ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka. Amin, amin, nawaambia, yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai. Maana kam avile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake. Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo; kwa maana sasa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu. Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.
Maoni
Ingia utoe maoni