Masomo ya Misa
Jumanne ya 3 ya Kwaresima (Jumanne, Machi 05, 2024)
Dan 3:25, 34-43
Ndipo Azaria akasimama akasali hivi, akifumbua kinywa chake katikati ya moto na kusema: Usituache kabisa, kwa ajili ya jina lako, wala usilitangue agano lako na kutuondolea rehema zako, kwa ajili ya Ibrahimu umpendaye, na kwa ajili ya Isaka mtumishi wako, na Israeli mtakatifu wako kama nyota za mbinguni na kama mchanga wao pwani. Maana sisi, Ee Bwana, tumekuwa duni kuliko mataifa yote, na kudhulumiwa leo katika ulimwengu wote kwa sababu ya dhambi zetu. Sasa hakuna mfalme wala nabii wala kiongozi; hakuna dhabihu wala kafara wala sadaka wala uvumba; wala mahali pa kukutolea dhabihu na kuona rehema. Lakini kwa moyo uliovunjika na kwa roho nyenyekevu tukubaliwe nawe, na sadaka yetu iwe machoni pako leo kama dhabihu za kondoo waume na ng’ombe, na kama kondoo wanono elfu kumi. Nasi tukufuate kwa unyofu, maana wanaokutumaini Wewe hawataaibika. Na sasa tunakufuata kwa moyo wote; tunakucha na kuutafuta uso wako. Usitufedheheshe, bali ututendee kwa kadiri ya fadhili zako, sawasawa na wingi wa huruma zako. Utuokoe kwa kadiri ya maajabu yako, na kulitukuza jina lako, Ee Bwana.
Zab 25:4-9
Ee Bwana unijulishe njia yako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.
(K) Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako.
Ee Bwana kumbuka rehema zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu,
Wala maasi yangu.
Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako.
(K) Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako.
Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake.
(K) Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako.
Yn 11:25, 26
Mimi ndimi ufufuo na uzima, asema Bwana; Yeye aniaminiye mimi, hatakufa kabisa na milele.
Mt 18:21-35
Petro alimwendea Yesu akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia; akamkamata, akamshika koo, akisema, Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nimekusamehe wewe deni ile yoe, uliponisihi; nawe pia haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapolipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehekwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.
Maoni
Ingia utoe maoni