Ijumaa. 03 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 2 ya Kwaresima (Jumanne, Februari 27, 2024)  

Somo la 1

Isa 1:10, 16-20

Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; achene kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.

Wimbo wa Katikati

Zab 50:8-9, 16-17, 21, 23

Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele yangu daima.
Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
Wala beberu katika mazizi yako.
(K) Autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wangu.

Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.
(K) Autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wangu.

Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza,
Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe,
Atoaye dhabihu za kushukuru, ndiye anayenitukuza.
Naye autengenezaye mwenyendo wake,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
(K) Autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wangu.

Shangilio

Mt 4:17

Tubuni asema Bwana, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.

Injili

Mt 23:1-12

Yesu aliwaambia makutano na wanafunzi wake, akasema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yoyote watakayowaambia, myashike, na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupapanua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi. Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na yeyote atakayejikweza atadhiliwa; na yeyote atakayejidhili atakwezwa.

Maoni


Ingia utoe maoni