Jumamosi. 04 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 2 ya Kwaresima (Jumatatu, Februari 26, 2024)  

Somo la 1

Dan 9:4–10

Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.

Wimbo wa Katikati

Zab 79:8–9, 11, 13

Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima,
Kwa maana tumedhilika sana.
(K) Usitutende sawasawa na hatia zetu, Ee Bwana.

Ee Mungu wokovu wetu utusaidie.
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofiri dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako.
(K) Usitutende sawasawa na hatia zetu, Ee Bwana.

Kuugua kwake aliyefungwa na kuingia mbele zako.
Kwa kadiri ya uweza wa mkono wako.
Uwahifadhi wana wa mauti.
Na sisi tulio watu wako, na kondoo za malisho yako,
Tutakushukuru milele;
Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi.
(K) Usitutende sawasawa na hatia zetu, Ee Bwana.

Shangilio

Mt 4:4

Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

Injili

Lk 6:36:38

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu kitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifruani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.

Maoni


Ingia utoe maoni