Jumamosi. 04 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 1 ya Kwaresima (Jumamosi, Februari 24, 2024)  

Somo la 1

Kumb 26:16-19

Musa aliwaambia watu: Leo hivi akuamuru Bwana, Mungu wako, kuzifanya amri hizi na hukumu; basi uzishike na kuzifanya kwa moyo wako wote na roho yako yote. Umemwungama Bwana leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake; naye Bwana amekuungama hivi leo kuwa taifa iliyotengwa iwe yake yeye, kama alivyokuahidi, na kuwa yakupasa kushika maagizo yake yote; na kuwa atakutukuza juu ya mataifa yote aliyoyafanya kwa sifa, na jina na heshima, nawe upate kuwa taifa takatifu kwa Bwana Mungu wako, kama alivyosema.

Wimbo wa Katikati

Zab 119:1-2, 4-5, 7-8

Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote.
(K) Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana.

Wewe umetuamuru mausia yako,
Ili sisi tuyatii sana.
Ningependa njia zangu ziwe thabiti,
Nizitii amri zako.
(K) Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana.

Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo,
Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako.
Nitazitii amri zako,
Usiniache kabisa.
(K) Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana.

Shangilio

Amo 5:14

Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi, hivyo Bwana, atakuwa pamoja nanyi.

Injili

Mt 5:43-48

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yetu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu? Hata watoza ushuru; je! Nao hawafanyi yay ohayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Maoni


Ingia utoe maoni