Jumanne. 07 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 6 ya Mwaka (Jumanne, Februari 13, 2024)  

Somo la 1

Yak 1:12-18

Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao. Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike. Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.

Wimbo wa Katikati

Zab 94:12-15, 18-19

Ee Bwana, heri mtu yule umwadhibuye na kumfundisha,
Kwa sheria yako;
Mpate kumstarehesha siku ya mabaya.
(K) Ee Bwana, heri mtu yule uliyemfundisha.

Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake,
Wala hutauacha urithi wake,
Maana hukumu itairejea haki,
Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata.
(K) Ee Bwana, heri mtu yule uliyemfundisha.

Niliposema, mguu wangu unateleza;
Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza.
Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu,
Faraja zako zaifurahisha roho yangu.
(K) Ee Bwana, heri mtu yule uliyemfundisha.

Shangilio

Yn 14:23

Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu, na baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake.
Aleluya.

Injili

Mk 8:14–21

Wafuasi wake Yesu walisahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu. Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode. Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate. Naye Yesu akatambua, akawaambia, Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito? Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? Wala hamkumbuki? Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili. Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande? Wakamwambia, Saba. Akawaambia, Hamjafahamu bado?

Maoni


Ingia utoe maoni