Masomo ya Misa
Kumbuku ya Mt. Scholastica, Bikira (Jumamosi, Februari 10, 2024)
1Fal 12:26-32; 13:33-34
Yeroboamu alisema moyoni mwake: Basi ufalme utairudia nyumba ya Daudi. Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya Bwana huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu hawa itamrudia bwana wao, yaani Rehoboamu, mfalme wa Yuda; nao wataniua mimi, na kumrudia Rehoboamu, mfalme wa Yuda. Kwa hiyo mfalme akafanya shauri, akafanyiza ng’ombe wawili wa dhahabu, akawaambia watu, Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri. Akamweka mmoja katika Betheli, na wa pili akamweka katika Dani. Jambo hili likawa dhambi, maana watu walikwenda kuabudu mbele ya kila mmoja, hata huko Dani. Tena akafanya nyumba za mahali pa juu, akafanya na watu wowote, watu wasio wa wana wa Lawi, kuwa makuhani. Yeroboamu akaamuru kushika sikukuu katika mwezi wa nane, siku ya kumi na tano ya mwezi, mfano wa sikukuu iliyokuwa katika Yuda, akapanda juu ili kuiendea madhabahu. Akafanya vivyo katiak Betheli akiwatolea dhabihu wale ng’ombe aliowafanya; akawaweka katika Betheli wale makuhani wa mahali pa juu alipokuwa amepafanya. Baada ya hayo Yeroboamu hakuiacha njia yake mbovu, lakini akafanya tena makuhani wa mahali pa juu, wa watu wowote. Kila aliyetaka akamfanya wakfu, ili wawepo makuhani wa mahali pa juu. Jambo hilo likawa dhambi kwa nyumba ya Yeroboamu, hata kuiharibu, na kuifuta usoni pa nchi.
Zab 106:6-7, 19-22
Tumetenda dhambi pamoja na baba zetu,
Tumetenda maovu, tumefanya ubaya.
Baba zetu katika Misri
Hawakufikiri matendo yako ya ajabu.
(K) Ee Bwana, unikumbuke mimi, kwa kibali uliyonayo kwa watu wako.
Walifanya ndama huko Horebu,
Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
Wakaubadili utukufu wao
Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani.
(K) Ee Bwana, unikumbuke mimi, kwa kibali uliyonayo kwa watu wako.
Wakamsahau Mungu mwokozi wao,
Aliyetenda makuu katika Misri:
Matendo makuu katika nchi ya Hamu,
Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.
(K) Ee Bwana, unikumbuke mimi, kwa kibali uliyonayo kwa watu wako.
Mt 4:4
Aleluya, aleluya,
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Aleluya.
Mk 8:1–10
Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akawaambia, Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula; nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali. Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani? Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba. Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake waaandikie; wakawaaandikia mkutano. Walikuwa na visamaki vichache; akavibariki, akasema wawaandikie na hivyo pia. Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate makanda saba. Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga. Mara akapanda chomboni pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha.
Maoni
Ingia utoe maoni