Jumanne. 16 Julai. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 5 ya Mwaka (Alhamisi, Februari 08, 2024)  

Somo la 1

1Fal 11:4-13

Mfalme Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni. Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake. Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu. Basi Bwana akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili, akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru Bwana. Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako. Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako. Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.

Wimbo wa Katikati

Zab 106:3-4, 35-37, 40

Heri washikao hukumu, Na kutenda haki sikuzote.
Ee Bwana, unikumbuke mimi,
Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
Unijilie kwa wokovu wako,
(K) Ee Bwana utukumbuke kwa kibali uliyonayo kwa watu wako.

Bali walijichanganya na mataifa,
Wakajifunza matendo yao.
Wakazitumikia sanamu zao,
Nazo zikawa mtego kwao.
(K) Ee Bwana utukumbuke kwa kibali uliyonayo kwa watu wako.

Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani.
Hasira ya Bwana ikawaka juu ya watu wake,
Akauchukia urithi wake.
(K) Ee Bwana utukumbuke kwa kibali uliyonayo kwa watu wako.

Injili

Mk 7:24-30

Yesu aliondoka Nazareti akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika. Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake. Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake. Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa. Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto. Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako. Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka.

Maoni


Ingia utoe maoni