Masomo ya Misa
Dominika ya 5 ya Mwaka (Jumapili, Februari 04, 2024)
Ayu 7:1-4, 6-7
Ayubu alianza kusema, Je! Mtu hana wakati wake wa vita juu ya nchi? Na siku zake, je! Si kama siku za mwajiriwa? Kama mtumishi atamaniye sana kile kivuli, Kama mwajiriwa anayetazamia mshahara wake; Ni vivyo nami nimepewa miezi ya ubatili iwe fungu langu, Nami nimeandikiwa masiku yenye kuchokesha. Hapo nilalapo chini, nasema, Nitaondoka lini? Lakini usiku huwa mrefu; Nami nimejawa na kujitupa huku na huku hata kupambazuke. Siku zangu hupita upesi kuliko chombo cha kufumia, Nazo zapita pasipokuwa na matumaini. Kumbuka ya kwamba maisha yangu ni upepo; Jicho langu halitaona mema tena.
Zab 147:1-6
Haleluya. Msifuni Bwana;
Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu,
Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri.
Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu,
Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli.
(K)Msifuni Bwana, huwaponya waliopondeka moyo
Huwaponya waliopondeka moyo,
Na kuziganga jeraha zao.
Huihesabu idadi ya nyota,
Huzipa zote majina.
(K)Msifuni Bwana, huwaponya waliopondeka moyo
Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu,
Akili zake hazina mpaka.
Bwana huwategemeza wenye upole,
Huwaangusha chini wenye jeuri.
(K)Msifuni Bwana, huwaponya waliopondeka moyo
1Kor 9:16-19, 22-23
Ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili. Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili. Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi. Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine.
Yn 8:12
Aleluya, aleluya
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, Yeye anifuataye atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya
Mk 1:29-39
Yesu na wafuasi wake walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko. Simoni na wenziwe wakamfuata; nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta. Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea. Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo.
Maoni
Ingia utoe maoni