Jumatatu. 13 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 4 ya Mwaka (Alhamisi, Februari 01, 2024)  

Somo la 1

1Fal 2:1-4, 10-12

Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako; ili Bwana afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli. Basi Daudi akalala na babaze, akazikwa mjini mwa Daudi. Na siku alizotawala Daudi juu ya Israeli zilikuwa miaka arobaini; huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu. Basi Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba yake; na ufalme wake ukawa imara sana.

Wimbo wa Katikati

1Nya 29:10-12

Uhimidiwe, Ee Bwana, Mungu wa Israeli baba yetu,
milele na milele.
(K) Bwana watawala juu ya vyote

Ee Bwana, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi;
(K) Bwana watawala juu ya vyote

Ee Bwana, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote.
Utajiri na heshima hutoka kwako wewe,
(K) Bwana watawala juu ya vyote

Mkononi mwako mna uweza na nguvu;
tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote.
(K) Bwana watawala juu ya vyote

Injili

Mk 6:7-13

Yesu aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu; akasema, Msivae kanzu mbili. Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung'uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao. Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.

Maoni


Ingia utoe maoni