Masomo ya Misa
Dominika ya 4 ya Mwaka (Jumapili, Januari 28, 2024)
Kum 18:15-20
Bwana, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye. Kama vile ulivyotaka kwa Bwana, Mungu wako, huko Horebu, siku ya kusanyiko, ukisema, wako, huko Horebu, siku ya kusanyiko, ukisema, Nisisikie tena sauti ya Bwana, Mungu wangu, wala nisiuone tena moto huu mkubwa, nisije nikafa. Bwana akaniambia, Wametenda vema kusema walivyosema. Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamburu. Hata itakuwa, mtu aisyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake. Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa.
Zab 94:1-2, 6-9
Njoni tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi.
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake. Msifanye migumu mioyo yenu.
Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake.
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake. Msifanye migumu mioyo yenu.
Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ile Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu.
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake. Msifanye migumu mioyo yenu.
1Kor 7:32-35
Wapendwa, nataka msiwe na masumbufu. Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendezeje Bwana; bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe. Tena iko tofauti hii kati ya mke na mwanamwali. Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana, apate kuwa mtakatifu mwili na roho. Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mumewe. Nasema hayo niwafaidie; si kwamba niwategee tanzi, bali kwa ajili ya vile vipendezavyo, tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine.
Yn 15:15
Aleluya, aleluya,
Siwaiti tena watumwa; Kwa maana mtumwa hajui atendalo Bwana wake, Lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
Mk 1:21-28
Yesu na wafuasi wake walishika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato Yesu akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.
Maoni
Ingia utoe maoni