Masomo ya Misa
Jumamosi ya 3 ya Mwaka (Jumamosi, Januari 27, 2024)
2Sam 12:1-7, 10-17
Bwana alimtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana-kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Hata msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng’ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfilia, bali alimnyang’anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikilia. Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma. Basi, Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. Bwana asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, anmi nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili. Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua. Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za Bwana nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa. Naye Nathani akatoka kwenda nyumbani kwake. Basi Bwana akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi, naye akawa hawezi sana. Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala usiku kucha chini. Nao wazee wa nyumba yake wakondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao.
Zab 51:10-15
Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako takatifu usiniondolee.
(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.
Unirudishie ya wokovu wako,
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
Nitawafundisha wakosaji njia zako,
Na wenye dhambi watarejea kwako.
(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.
Ee Mungu, Mungu wa wokovu wangu,
Uniponye na damu za watu,
Na ulimi wangu utaiimba haki yako.
Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa changu kitazinena sifa zako.
(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.
Yn 3:16
Aleluya, aleluya,
Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele.
Aleluya.
Mk 4:35-41
Siku ile kulipokuwa jioni, Yesu akawambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna Imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?
Maoni
Ingia utoe maoni